Ubalozi kwa kushirikiana na taasisi ya Bezos Earth Fund uliandaa mkutano wa Mabalozi (Ambassadorial Briefing) wa nchi za Afrika hapa Washington, D.C., kwa lengo la kupeana taarifa kuhusu maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Afrika kuhusu Nishati utakaofanyika tarehe 27 - 28 Januari 2025 jijini Dar es Salaam. Mkutano huo uliwahusisha pia Viongozi Waandamizi wa Benki ya Dunia wakiwemo Makamu wa Rais wa Benki hiyo, Bi. Victoria Kwakwa na Bw. Ousmane Diagane na Wakurugenzi Watendaji wa Benki hiyo. Washiriki wengine walitoka taasisi za Bezos Earth Fund, wakiongozwa na Sir. Andrew Steer, Rais na Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo; taasisi ya Rockefeller, wakiongozwa na Dr. Raj Shah, Rais wa taasisi hiyo; na Viongozi wa vyama vya wafanyabiashara na taasisi za tafiti (think tanks). Mkutano wa Wakuu wa Nchi utakaofanyika jijini Dar es Salaam utaleta pamoja wadau muhimu wa sekta ya nishati ili kujadili mikakati ya kufikisha nishati ya umeme kwa Waafrika Milioni 300 hadi kufika mwaka 2030 (Mission 300).