Mhe. Dkt. Godwin Mollel (Mb.), Naibu Waziri wa Afya ameongoza Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa masuala ya saratani ulioandaliwa na taasisi ya Global Health Catalyst (GHC) ya hapa Marekani. Mkutano huo uliofanyika jijini Washington, D.C., umewakutanisha wadau wa masuala ya saratani kwa lengo la kujadili njia na mbinu mbalimbali za kupambana na ugonjwa huo na kuhimiza ushirikiano katika mapambano hayo. Katika mkutano huo, Tanzania ilipata fursa ya kueleza changamoto, mafanikio na hatua mbalimbali ambazo Serikali inachukua katika kupambana na ugonjwa wa saratani. Pia, ilieleza kuhusu Kituo cha Umahiri cha Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Saratani kinachoanzishwa jijini Dodoma kwa kushirikiana na taasisi ya GHC, kwa lengo la kuhimiza wadau kuunga mkono uanzishwaji wa Kituo hicho. Aidha, Tanzania ilipewa tuzo kutambua mchango wa Serikali kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa huo.