Ubalozi ulishirikiana na taasisi iitwayo World Artists Experiences (WAE) kuandaa tamasha kwa njia ya mtandao lililoonesha filamu ya Tanzania: the Royal Tour kwa wadau wa taasisi hiyo.  Mhe. Balozi Dkt. Elsie Sia Kanza alikuwa mgeni rasmi kwenye tamasha hilo ambapo alitoa hotuba ya ufunguzi iliyoelezea vivutio vya kipekee vya utalii vinavyopatikana Tanzania, utamaduni wake mzuri na ukarimu wa watu wake, na hivyo aliwakaribisha washiriki wa Tamasha hilo kuitembelea Tanzania. Kadhalika, Mhe. Balozi alijibu maswali mbalimbali kutoka kwa washiriki waliokuwa na shauku ya kufahamu zaidi kuhusu utalii, utamaduni na historia ya Tanzania.

Mtengenezaji wa filamu hiyo, Bw. Peter Greenberg alishiriki pia kwenye Tamasha hilo kwa kuelezea kwa kifupi kuhusu filamu husika na vivutio vizuri vya utalii alivyovishuhudia Tanzania.

WAE ni taasisi isiyo ya kiserikali ya hapa Marekani iliyojikita katika kuleta uelewa wa tamaduni za sehemu mbalimbali duniani kwa vyuo, shule na jamii ya Wamarekani.

Filamu ya Tanzania: The Royal Tour ndiyo pekee kutoka nchi za Kiafrika inayooneshwa kwenye tamasha hilo kwa mwaka huu, 2025.