Ubalozi umeshiriki katika Mkutano wa Biashara Afrika (Africa Business Conference) ulioandaliwa na Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Harvard jijini Boston, Massachusetts. Mhe. Balozi Dkt. Elsie Sia Kanza alikuwa ni miongoni mwa wanajopo kwenye mjadala kuhusu mustakabali wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).
Pamoja na masuala mengine, Mhe. Balozi alieleza kwenye Mkutano huo kuwa Tanzania inaendelea kushirikiana na nchi nyingine wanachama wa AfCFTA na wadau wengine katika ujenzi wa miundombinu ya kikanda na uboreshaji wa sera za kibiashara kwenye sekta za kipaumbele ikiwemo ujenzi,uchukuzi, nishati, afya na forodha. Kwa ujumla wake, Mkutano ulijadili kuwa ili kufikia malengo ya kuanzishwa kwake, nchi wanachama wa AfCFTA zinashauriwa kuongeza uwekezaji wa miundombinu wezeshi, kuongeza kasi ya kuondoa vikwazo vya kikodi na visivyo vya kikodi na kuvutia uanzishwaji wa minyororo ya thamani ndani ya bara la Afrika.
Aidha, pembezoni mwa mkutano huo, Mhe. Balozi alikutana na kufanya mazungumzo na Watanzania waliowahi kusoma na ambao bado wanasoma katika vyuo vikuu mbalimbali vya hapa Marekani walioshiriki kwenye Mkutano tajwa, ikiwemo Harvard, MIT na Stanford. Mhe. Balozi alitoa rai kwa Watanzania hao kushirikiana na Ubalozi katika masuala mbalimbali muhimu kwa maendeleo ya Tanzania, na Watanzania hao walieleza pia utayari wao kushirikiana na Ubalozi kwa manufaa ya Taifa.



