Ubalozi unashiriki kwenye kongamano liitwalo Maendeleo ya Uchumi (Tanzania Economic Development Summit) linalofanyika kuanzia tarehe 10 hadi 14 Machi 2025, katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam. Kongamano hilo limeandaliwa na Ubalozi na taasisi ya National Institute of Minority Economic Development (NIMED) ya nchini Marekani kwa kushirikiana na taasisi ya Sister Cities International (SCI) pia ya Marekani na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade).
Kongamano hili limewezesha wafanyabiashara wa Tanzania na Marekani pamoja Viongozi na Wawakilishi wa Serikali za nchi hizo mbili kujadili fursa za biashara na uwekezaji katika sekta za kilimo, viwanda, elimu na nyumba. Kongamano pia limetoa fursa kwa baadhi ya wafanyabiashara ya Tanzania kuonesha bidhaa wanazozalisha na wafanyabiashara wa Marekani kutembelea Zanzibar na kampuni za Africab, Kamal na Kazi Yetu zilizopo jijini Dar es Salaam.
Kongamano hilo limehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali wakiongozwa na Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Mashariki; Mhe. Shariff A. Shariff, Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais- Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar; Mhe. Exaud Kigahe (Mb.), Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara; Mhe. Dkt. Elsie S. Kanza, Balozi wa Tanzania nchini Marekani; na Mhe. Andrew Lentz, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania.



