Kufuatia mwaliko kutoka kwa uongozi wa Makanisa ya Umoja ya hapa Marekani, Ubalozi ulishiriki kwenye Kongamano la Dini na Mahafali ya Chuo cha Kimataifa cha Biblia cha Umoja (Umoja International Bible College) kuanzia tarehe 07 hadi 09 Machi 2025, jijini Dallas, Texas. Kongamano hilo ambalo hukutanisha diaspora wa Tanzania na wa Mataifa mengine yanayozungumza Kiswahili na wageni kutoka Tanzania, ndilo Kongamano kubwa zaidi la kidini linaloendeshwa kwa lugha ya Kiswahili hapa Marekani, hivyo, pamoja na kuwaleta pamoja diaspora, husaidia pia kukuza na kuitangaza lugha yetu adhimu. Mwakilishi wa Ubalozi kwenye Kongamano hilo, Bi. Sophia V. Gunda aliwasilisha salamu kwa niaba ya Mhe. Balozi ambapo pamoja na masuala mengine, alisisitiza mshikamano baina ya diaspora, alitambua mchango wao kwenye maendeleo ya nchi yetu, pia aliwaomba kuiombea nchi yetu pamoja na Viongozi wake.