Mhe. Balozi Dkt. Elsie S. Kanza ameshiriki kwenye Jopo lililojadili kuhusu mazingira ya biashara barani Afrika kufuatia mabadiliko yanayoendelea kwenye nchi mbalimbali yenye mwelekeo wa kulinda zaidi biashara zao za ndani. Mjadala huo uliandaliwa na Shule ya Mambo ya Nje ya Chuo Kikuu cha Amerika (American University), hapa Washington, D.C.
Kwenye mchango wake, pamoja na masuala mengine, Mhe. Balozi ameeleza kuwa kutokana na mazingira hayo ya kibiashara, ni muhimu kwa nchi za Kiafrika kuimarisha biashara baina yao kupitia Jumuiya zao za Kikanda (RECs) na Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) pamoja na kupanua wigo wa nchi wanazofanya nazo biashara ndani na nje ya Afrika. Pia, Mhe. Balozi amesisitiza umuhimu wa Mpango wa AGOA kuongezwa muda ili kuimarisha uhusiano wa kibiashara baina ya nchi za Afrika na Marekani, hasa kwa kuzingatia kuwa Mpango huo una manufaa kwa pande zote mbili.
Washiriki wengine kwenye jopo hilo lililoongozwa na Prof. Carl LeVan wa Chuo tajwa, walikuwa ni Bi. Florie Liser, Rais na Mkurugenzi Mkuu wa taasisi ya kibiashara ya Corporate Council on Africa (CCA) ya hapa Marekani na Bi. Natalie Hanson, Kiongozi na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Textile Trade Solutions ya Marekani.



