Serikali ya Tanzania imeingia makubaliano ya ushirikiano na Taasisi ya Bioventure for Global Health (BVGH) ya nchini Marekani ili kuimarisha huduma za Saratani nchini Tanzania.
Makubaliano hayo yamefikiwa Julai 16, 2024 katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania Jijini Washington DC nchini Marekani na kushuhudiwa na Waziri wa Afya wa Tanzania Mhe. Ummy Mwalimu (Mb) na Mheshimiwa Dkt. Elsie Sia Kanza, Balozi wa Tanzania nchini Marekani.
Ushirikiano huo kati ya Wizara ya Afya na Taasisi hiyo, unalenga kuimarisha huduma kwa kutoa fursa za mafunzo kwa watalaam wa saratani wakiwemo madaktari Bingwa na wabobezi katika huduma za mionzi.
Aidha mradi huo pia utatoa fursa kwa ajili ya tafiti katika huduma za Saratani, kuimarisha miundo mbinu ya huduma za saratani na kuwezesha upatikanaji wa dawa za saratani kwa gharama nafuu kwa watanzania.
Akiongea baada ya kusainiwa makubaliano hayo, Waziri wa Afya amesema Serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais dkt Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuboresha huduma za Saratani zinapatikana kwa urahisi kwa watanzania ili kupunguza vifo vitokanavyo na Saratani.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya BVGH Bi. Jennifer Bent baada ya kusaini makubaliano hayo alielezea kufurahishwa kwake na utayari wa Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi hiyo pamoja na namna ambavyo serikali imedhamiria kukabiliana na ugonjwa huu wa Saratani nchini.