Ubalozi kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway na taasisi ya Clean Cooking Alliance umeitisha mkutano kuhusu nishati safi ya kupikia kwa ajili ya jumuiya ya hapa Marekani. Mkutano huo uliohusisha wadau mbalimbali wakiwemo wawakilishi wa Serikali ya Marekani, jumuiya ya kidiplomasia, mashirika na taasisi za kimataifa, taasisi za tafiti na taasisi zisizo za kiserikali ulilenga kuendeleza kasi na ari ya Mkutano wa Kimataifa wa Nishati Safi ya Kupikia kwa Afrika uliofanyika Paris, Ufaransa chini ya uenyekiti wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Waziri Mkuu wa Norway; Rais AfDB; na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya IEA. 
Mhe. Balozi Dkt. Elsie S. Kanza alieleza washiriki kuhusu Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia na jitihada nyingine zinazofanywa na Serikali katika kukuza ajenda hiyo. Aidha, Mhe. Balozi alitoa rai kwa washiriki kuunga mkono ajenda ya nishati safi ya kupikia kutokana na umuhimu wake kwa afya za binadamu, maendeleo ya watu, kuwainua wanawake na mustakabali wa dunia.