Mhe. Balozi Dkt. Elsie S. Kanza alikuwa ni miongoni mwa wazungumzaji kwenye mkutano wa wadau wa uwekezaji wa Marekani kwenye sekta za madini na nishati barani Afrika. Kwenye mkutano huo, washiriki walipata fursa ya kujadili namna bora ya kuchochea uwekezaji wa sekta binafsi kwenye sekta hizo mbili.

Akitoa mchango wake kwenye mkutano huo, pamoja na masuala mengine, Mhe. Balozi Kanza alieleza fursa za uwekezaji zinazopatikana Tanzania kwenye sekta husika pamoja na mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji yaliyopo yanayotokana na mageuzi yanayoendelea kwenye eneo hilo. Mhe. Balozi alizialika pia kampuni za biashara kutoka Marekani kuwekeza nchini Tanzania kwenye sekta hizo.

Mkutano huo ulioratibiwa na taasisi ya tafiti (think tank) ya Center for Strategic and International Studies (CSIS), ulihudhuriwa na Wanadiplomasia, Wawakilishi wa Serikali na Sekta binafsi ya Marekani pamoja na wawakilishi kutoka Vyuo Vikuu na taasisi nyingine mbalimbali.