Ubalozi kwa kushirikiana na shirika la International Cotton Advisory Committee (ICAC) lenye makao makuu hapa Washington, D.C., uliandaa mkutano wa wadau wakuu wa sekta ya pamba na nguo nchini Tanzania. Mkutano huo umewezesha wadau kujadili fursa zilizopo kwenye minyororo ya thamani ya viwanda vya kuzalisha bidhaa mbalimbali za nguo na kuweka mikakati ya kuchochea uzalishaji wa bidhaa hizo. Mkutano pia ulijadili namna ya kuweka mikakati thabiti ya kuiwezesha Tanzania  kuimarisha minyororo yake ya thamani ya nguo na mavazi ili kunufaika zaidi na soko la nguo la Marekani, ambalo ni soko kubwa zaidi duniani.

Itakumbukwa kuwa zaidi ya 95% ya mauzo ya Tanzania nchini Marekani kupitia mpango wa AGOA ni bidhaa za nguo na kuna fursa kubwa zaidi kwa Tanzania kuendelea kunufaika na soko hilo.

Mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao ulihudhuriwa na viongozi na maafisa waandamizi kutoka Wizara na taasisi mbalimbali za Serikali, sekta binafsi ikiwemo vyama vya wafanyabiashara na taasisi za elimu ya juu.