Mhe. Balozi Dkt. Elsie S. Kanza ameshiriki kwenye maonesho ya 54 ya uwindaji ya Safari Club International Convention (SCI) yaliyofanyika jijini Nashville, Tennessee, kuanzia tarehe 18 hadi 21 Februari 2026. Maonesho hayo yaliwakutanisha wadau wa uwindaji kutoka sehemu mbalimbali duniani. Aidha, maonesho ya SCI hufanyika sambamba na vikao vya kitaalamu vya masuala ya uwindaji vinavyohusisha kampuni za uwindaji, mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali pamoja na wanachama wa SCI.
Takribani kampuni 15 za uwindaji wa kitalii kutoka Tanzania zilishiriki katika maonesho hayo. Ikumbukwe kuwa Marekani ndiyo nchi inayoongoza kwa kuleta wawindaji wengi zaidi nchini Tanzania.
Aidha, pembezoni mwa maonesho hayo, Mhe. Balozi alifanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wakiwemo kutoka Serikali ya Marekani, Bunge la Marekani na wadau wengine wa masuala ya uwindaji. Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano katika masuala ya uhifadhi, uwindaji endelevu na kubadilishana uzoefu kuhusu sera na mifumo bora ya usimamizi wa rasilimali za wanyamapori.



