Mheshimiwa Balozi Dkt. Elsie Sia Kanza alikuwa mzungumzaji mkuu kwenye mkutano wa uwekezaji ulioandaliwa na Africa Global Chamber of Commerce, jijini Chicago, Illinois. Mkutano huo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Ubalozi wa kushirikiana na wadau mbalimbali katika ngazi ya majiji na majimbo, kwa lengo la kutangaza fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania.

Katika mkutano huo, Mheshimiwa Balozi alielezea kwa kina utulivu wa mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini Tanzania, jitihada thabiti zinazochukuliwa na Serikali katika kuvutia uwekezaji, pamoja na fursa zilizopo katika sekta za kipaumbele. Aliwakaribisha washiriki kuitembelea Tanzania ili kujionea fursa hizo na kuzichangamkia.

Wawekezaji walioshiriki katika mkutano huo walionesha kuvutiwa na fursa zilizowasilishwa na kuonesha nia ya kufanya ziara ya kibiashara nchini Tanzania mwishoni mwa mwaka huu. Ziara hiyo itaratibiwa na Africa Global Chamber of Commerce kwa kushirikiana na Ubalozi.