UBALOZI WAADHIMISHA SIKU YA KISWAHILI DUNIANI

Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Marekani na Mexico, kwa kushirikiana na Africatown, African Cultural Alliance of North America (ACANA), ODUNDE 365 Festival, na The World Trade Center of Philadelphia, uliadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani tarehe 26 Julai 2026 jijini Philadelphia, Marekani.

Maadhimisho hayo yalihusisha kufanyika kwa maonesho ya mavazi, ngoma, muziki, uzinduzi wa kitabu "Twende kwa Bibi", bidhaa mbalimbali zenye asili ya Tanzania na maonesho ya chakula cha kiswahili kwa wageni walioshiriki.

Maadhimisho hayo yalilenga kuenzi na kuendelea kutangaza lugha, mila, desturi na utamaduni wa Kiswahili. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mhe. Kendy Alwarez, Meya wa Lewisburg; Bw. Stanley Straughter, Mwenyekiti wa Bodi ya Uchumi na Maendeleo ya Mji wa Africatown, na Donavan West, Mkurugenzi wa Roundtable Business akimwakilisha Meya wa Jiji la Philadelphia. Mhe. Balozi Musa Haji Ali, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa pamoja na Watanzania, wanadiaspora, marafiki wa Tanzania, na wasomi kutoka maeneo mbalimbali walishiriki.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Balozi Dkt. Elsie Kanza alimshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele kukitangaza na kukiendeleza Kiswahili. Alisema chini ya Serikali yake Mhe. Rais Samia amedhamiria kukikuza na kukiendeleza Kiswahili duniani kote.

Balozi Kanza alisisitiza watu kuendelea kujifunza Kiswahili maana ni lugha inayokuwa kwa kasi na kuwa Tanzania itaendelea kukitumia kama nyenzo ya kuimarisha diplomasia, uwekezaji, utalii, biashara na ushirikiano wa kimataifa. Kwa hapa Marekani zaidi ya Vyuo Vikuu 100 vinafundisha lugha ya Kiswahili.