Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb.) (wa sita kulia) akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Dkt. Elsie Kanza (wa saba kulia) pamoja na viongozi waandamizi wa Serikali ya Tanzania, amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Shirika la Changamoto za Milenia-MCC kutoka Marekani, ukiongozwa na Naibu Afisa Mtendaji Mkuu wake, Bi. Chidi Blyden (wa tano kulia).
Mhe. Dkt. Nchemba aliishukuru MCC kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya nchi ambapo kupitia Mradi wa Changamoto za Milenia uliotekelezwa nchini kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2008 hadi 2013, uliiwezesha Tanzania kupata dola za Marekani 698 milioni, zilizotumika kutekeleza miradi katika sekta za usafirishaji, nishati na maji.
Kwa upande wake, Naibu Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), Bi. Chidi Blyden, ameipongeza Tanzania kwa hatua kubwa ilizopiga katika kuimarisha masuala ya utawala bora, demokrasia na haki za binadamu chini ya utawala wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, hatua iliyolifanya Shirika lake kurejesha ushirikiano na Serikali.
Bi. Blyden alieleza kuwa Wataalam kutoka MCC wanaendelea na mijadala na wataalam wa Serikali ili kuharakisha kuanza kwa utekelezaji wa mpango huo ambao matokeo yake hapo baadae utaiwezesha Marekani kurejesha mradi wa Changamoto za Milenia (MCC-Compact) ambao utakuwa na lengo la kusaidia nchi kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ya maendeleo.
Mwezi Desemba mwaka 2023, Bodi ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), ilizichagua Tanzania na Philippines, kama wabia wake katika kuandaa programu za awali (threshold programs) zitakazolenga katika mageuzi ya kisera na kitaasisi ambazo nchi hizi zinaweza kuyafanya ili kupunguza umasikini na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Bodi hiyo ya MCC ilichukua uamuzi huo baada ya Tanzania na Ufilipino, kuonesha dhamira mpya ya kusukuma mbele mageuzi muhimu ya kuimarisha utawala wa kidemokrasia, kulinda haki za binadamu na kupambana na rushwa.
Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), ni shirika huru la Serikali ya Marekani linalojielekeza kupunguza umaskini duniani kupitia ukuaji wa kiuchumi, kwa kutoa ruzuku na misaada ya muda maalum kwa nchi zinazokidhi viwango na vigezo thabiti vya utawala bora, mapambano dhidi ya rushwa na kuheshimu haki za kidemokrasia.