Mhe. Balozi Dkt. Elsie S. Kanza alishiriki kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Norman E. Borlaug (World Food Prize International Dialogue 2025) uliofanyika Des Moines, Iowa. Mkutano huo uliwaleta pamoja viongozi, wanasayansi, wakulima na wadau wa sekta binafsi kujadili maendeleo ya kilimo, usalama wa chakula na lishe duniani.

Pembezoni mwa Mkutano huo, Mhe. Balozi alitembelea banda la The Outreach Program, Shirika Lisilo la Kiserikali linalotekeleza miradi ya maendeleo ya jamii nchini Tanzania ikiwemo inayohusu maji safi, huduma za afya, elimu na lishe kwa wanafunzi.

Vilevile, Mhe. Balozi alishiriki katika ziara maalumu ya mafunzo kwenye mashamba kwa ajili ya kujifunza mbinu za ukulima wa kisasa.

Pia, Mhe. Balozi alifanya mazungumzo na Mshindi wa mwaka 2025 wa Tuzo ya World Food Prize, Dkt. Mariangela Hungria kutoka Brazil na kujadili namna Tanzania inavyoweza kunufaika na tafiti za mshindi huyo wa Tuzo tajwa inayoheshimika kwenye sekta ya kilimo, katika kukuza uzalishaji na ubora wa mazao mbalimbali nchini Tanzania.