Mheshimiwa Balozi Dkt. Elsie S. Kanza ameshiriki kwenye kampeni maalum ya kushawishi mamlaka za nchi ya Marekani kurefusha muda wa kutekeleza programu AGOA iliyofanyika hapa Washington D.C., kuanzia tarehe 12 hadi 15 Januari 2026.
AGOA ni programu inayowezesha nchi wanufaika barani Afrika kuingiza bidhaa zenye sifa hapa Marekani bila kulipa ushuru. Mathalani, AGOA imechangia kwenye kasi ya ukuaji wa viwanda vya nguo barani Afrika kwani imewezesha nchi zinazonufaika na programu hiyo kuuza bidhaa za nguo hapa Marekani kwa bei ya ushindani. Kwa upande wa Tanzania, takwimu zinaonesha kuwa takribani asilimia 95 ya thamani ya bidhaa zote za Tanzania zinazoingia nchini Marekani chini ya programu ya AGOA, ni nguo.
Itakumbukwa kuwa tarehe 12 Januari 2026, Bunge la Wawakilishi la Marekani (U.S. House of Representatives) lilipitisha muswada wa kurefusha muda wa kutekeleza programu ya AGOA kwa miaka mitatu (3) kuanzia tarehe 30 Septemba, 2025 hadi tarehe 31 Desemba 2028. Ili muswada huo uanze kutumika, unapaswa kuungwa mkono na Bunge la Seneti la Marekani na kisha kutiwa saini na Rais wa Marekani. Hivyo, kwa sasa muswada huo umepelekwa kwenye Bunge la Seneti.
Kwenye kampeni hiyo, washiriki walipata fursa ya kukutana kwa mazungumzo na baadhi ya Wabunge wa Bunge la Marekani. Vinara wa kampeni hiyo ni wadau wa biashara ya nguo kutoka sekta binafsi barani Afrika na Marekani kwa kushirikiana na Balozi za nchi za Afrika zinazoongoza katika uuzaji wa nguo hapa Marekani. Sekta binafsi ya Tanzania iliwakilishwa na kampuni ya Tooku Tanzania ambayo inazalisha nguo jijini Dar es salaam.

