Mhe. Balozi Dkt. Elsie Sia Kanza alishiriki kwenye jopo lililojadili nafasi ya Mabalozi katika kutekeleza Diplomasia ya Sayansi ambalo lilikuwa ni sehemu ya Mkutano wa Diplomasia ya Sayansi (Science Diplomacy) ulioandaliwa na taasisi ya Science Diplomacy Hub ya Chuo Kikuu cha Johns Hopkins cha hapa Marekani. Mkutano huo ulikutanisha Mabalozi, wanadiplomasia, wanazuoni na viongozi mbalimbali wanaotekeleza sera za kisayansi.

Kwenye mchango wake, pamoja na masuala mengine, Mhe. Balozi alizungumzia namna Tanzania inavyoweka kipaumbele kwenye tafiti za kisayansi katika kutafuta majawabu ya changamoto tofauti na inafanya hivyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Alieleza pia kuwa tafiti hizo ni muhimu kwa maendeleo ya watu na nchi yetu na pia zinatoa mchango katika kutatua changamoto za kimataifa. Aidha, Mhe. Balozi alisisitiza umuhimu wa wadau kutoka nchi mbalimbali kushirikiana katika kuleta maendeleo ya kisayansi kwa manufaa ya wote.

Pamoja na Mhe. Balozi, wanajopo wengine walikuwa ni Mhe. Petra Schneebauer, Balozi wa Austria nchini Marekani na Mhe. Birgitta Tazelaar, Balozi wa Uholanzi nchini Marekani.