Mhe. Balozi Dkt. Elsie Sia Kanza alishiriki na kutoa hotuba maalum katika Mkutano wa 119 wa Chama cha Maafisa wa Fedha wa Serikali (Government Finance Officers Association – GFOA) uliofanyika hapa Washington, D.C. Chama hicho kina wanachama zaidi ya 20,000 kutoka nchini Marekani na Canada.

Aidha, katika hatua ya kipekee na ya kujivunia, Mkutano huo ulimchagua diaspora wa Tanzania, Bw. Lunda Asmani, CPFO kuwa Rais wa chama hicho.

Akihutubia Mkutano wa GFOA, Mhe. Balozi Kanza alimpongeza Bw. Lunda kwa kuaminiwa na kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo muhimu. Pia, aliwapongeza na kuwashukuru maafisa wa fedha kwa mchango wao mkubwa katika kuimarisha mifumo ya kifedha katika ngazi mbalimbali za serikali. Vilevile, alieleza juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuboresha sekta ya fedha kwa kupitia maboresho ya mifumo ya usimamizi wa fedha za umma, uwekezaji katika mifumo ya kidijitali ya fedha, kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma. Mhe. Dkt. Kanza alitumia fursa hiyo pia kuwaalika washiriki wa mkutano huo kutembelea Tanzania, akieleza vivutio mbalimbali vya kiutalii vinavyopatikana nchini.

Ubalozi unapenda kumpongeza tena Bw. Asmani, CPFO kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa GFOA.