Ubalozi uliratibu na kushiriki kwenye ziara ya Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (Mb.), Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Marekani ambako alimwakilisha Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sherehe za uzinduzi wa jengo jipya la maonesho ya sanaa za Afrika kwenye Makumbusho ya Metropolitan (the Met) jijini New York.
Kwenye uzinduzi huo, pamoja na masuala mengine, filamu maalum kuhusu urithi wa kihistoria wa miji ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara ilioneshwa kwa mara ya kwanza. Pia, Mhe. Waziri alifanya mazungumzo na Bw. Max Hollein, Mkurugenzi na Mtendaji Mkuu wa the Met na kukubaliana maeneo mbalimbali ya ushirikiano.
Akiwa New York, Mhe. Waziri Prof. Kabudi alifanya mazungumzo pia na Balozi Martin Kimani, Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Afrika (the Africa Center); Bi. Nabiya Syed, Mkurugenzi Mtendaji wa Mozilla Foundation na kujadili kuhusu Kiswahili na akili mnemba na pia alitembelea na kufanya mazungumzo na uongozi wa kampuni ya Tiffany & Co., ambayo ndiyo iliyatambulisha madini ya Tanzanite duniani mwaka 1968. Masuala mbalimbali ya ushirikiano yalijadiliwa kwenye mikutano hiyo.
The Met ni makumbusho makubwa zaidi kwa eneo kwenye mabara ya Amerika na ni ya 3 kwa ukubwa wa eneo duniani. Pia, makumbusho hayo yanaongoza kwa kutembelewa zaidi hapa Marekani na yanashika nafasi ya 5 kwenye orodha ya makumbusho ya sanaa yanayotembelewa zaidi duniani.


