Mhe. Balozi Dkt. Elsie Sia Kanza alishiriki kwenye mkutano na waandishi wa habari ulioitishwa na Mhe. Jonathan Jackson na Mhe. Sheila Cherfilus-McCormick, Wabunge wa Bunge la Wawakilishi la Marekani (U.S. House of Representatives) kwenye viwanja vya Bunge hilo hapa Washington, D.C. Mkutano huo uliitishwa kwa lengo la kuzungumzia Maadhimisho ya Siku ya Afrika (Africa Day) yanayofanyika tarehe 25 Mei kila mwaka. Mkutano pia ulisisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano baina ya Afrika na Marekani na ulitambua nafasi ya diaspora ya Afrika hapa Marekani katika kuimarisha uhusiano huo. Kwa ujumla wake, Mkutano ulilenga kuendelea kuiweka Afrika kwenye ajenda na mijadala ya umma wa Marekani, watunga sera wa Marekani, na wadau wengine muhimu.
Pamoja na Mhe. Balozi Kanza, wengine walioshiriki kwenye Mkutano huo ni Mabalozi wa nchi za Uganda na Tunisia; wawakilishi wa Balozi nyingine za Afrika; taasisi na wadau mbalimbali wanaojishughulisha na masuala ya Afrika.


