Mhe. Balozi Dkt. Elsie Sia Kanza ameshiriki kama mwanajopo kwenye Kongamano la Masuala ya Nishati ya Umeme Duniani lililoandaliwa na Taasisi ya Edson Electric Institute ya hapa Washington, D.C.
Akizungumza kwenye jopo hilo, Mhe. Balozi alieleza kuhusu jitihada thabiti za Serikali za kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi na umeme wa uhakika na gharama nafuu kwa wananchi wote. Mhe. Balozi alieleza kuwa miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati uliofanyika Januari 2025 jijini Dar es Salaam na kutoa fursa kwa nchi za Afrika na washirika mbalimbali kuahidi kushirikiana kutatua changamoto ya upatikanaji wa nishati ya umeme Afrika; uzinduzi wa Mpango Mahsusi wa Kitaifa kuhusu Nishati (National Energy Compact). Jitihada nyingine ni pamoja na utekelezaji wa miradi ya kitaifa na kikanda ya kuzalisha, kusafirisha na kuunganisha umeme pamoja na maboresho ya Sera za biashara ya umeme kikanda.
Pia, Mhe. Balozi alibainisha fursa zinazopatikana kwenye sekta ya nishati nchini Tanzania na kukaribisha sekta binafsi kuzichangamkia. Katika hilo, Mhe. Balozi alieleza kuwa kwa sasa Tanzania inazalisha umeme wa kutosha na Serikali ipo tayari kushirikisha Sekta binafsi katika ujenzi wa njia za kusafirisha umeme wa msongo mkubwa kwa ajili ya mahitaji ya soko la ndani ya nchi, kanda za Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Wanajopo wengine walioshiriki pamoja na Mhe. Balozi Kanza walikuwa ni Mhe. Jesper Møller Sørensen, Balozi wa Denmark nchini Marekani; na Bw. Mungo Woodfield, Afisa Mwandamizi wa Ubalozi wa Uingereza.


