Mheshimiwa Balozi alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya miaka 25 ya uhusiano wa majiji dada (sister city relationship) kati ya Moshi na Delray Beach, Florida. Maadhimisho hayo yalihudhuriwa pia na Meya wa jiji la Delray Beach, Mhe. Tom Carney; Seneta Mark Barnard wa Bunge la Seneti la Florida; Viongozi mbalimbali wa jiji la Delray Beach; Viongozi wa taasisi ya Sister Cities ya Delray Beach na miji mingine ya Florida; waanzilishi wa uhusiano baina ya Moshi na Delray Beach; Viongozi wa Chemba ya Biashara ya jiji la Delray Beach; diaspora wa Tanzania; na wananchi wa Delray Beach na miji mingine ya jirani.
Akihutubia kwenye maadhimisho hayo, pamoja na kuipongeza miji hiyo kwa kuadhimisha miaka 25 ya uhusiano wa miji dada, Mhe. Balozi aliitaka miji hiyo kuendelea kuimarisha uhusiano huo na kuufanya ulete manufaa zaidi ya kiuchumi, kibiashara, kielimu na maeneo mengine muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Mhe. Balozi alitumia pia fursa hiyo kuwakaribisha washiriki kutembelea Tanzania kwa ajili ya kutalii na kutafuta fursa za biashara na uwekezaji.


