Tarehe 13 Agosti 2025, Mheshimiwa Balozi Dkt. Elsie S. Kanza alikutana na kufanya mazungumzo na Mstahiki Meya wa jiji la Durham, Mhe. Leonardo Williams kwa ajili ya kudumisha na kustawisha uhusiano uliopo kwa muda mrefu baina ya Durham na Tanzania. Mathalani, jiji la Durham na jiji la Arusha ni majiji dada (sister cities) kwa zaidi ya miaka 30. Kadhalika, kumekuwa na ushirikiano mzuri wa takribani miaka 20 baina ya Chuo Kikuu cha Duke kilichopo Durham na Hospitali ya KCMC ya Moshi unaojikita kwenye masuala ya elimu, tafiti na utoaji wa huduma za afya.

Kwenye Mkutano huo, pamoja na masuala mengine, Mhe. Balozi Kanza na Mstahiki Meya Williams walieleza utayari wao wa kuongeza msukumo kwenye uhusiano wa kiabishara ikiwemo kwenye sekta za nishati na madini adimu kwa kuzingatia nafasi ya Durham kwenye Ukanda wa Betri wa Marekani, na aina ya madini yanayopatikana nchini Tanzania na dhamira ya Serikali ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uchakataji madini barani Afrika.

Ustawishaji wa ushirikiano hadi kwenye ngazi majiji na majimbo ni sehemu ya mkakati wa Ubalozi wa kupanua na kuchangamkia fursa za kibiashara, uwekezaji na za kijamii hapa Marekani.