Mheshimiwa Balozi Dkt. Elsie S. Kanza amekutana kwa mazungumzo na Bw. Eric Trachtenberg, Mkurugenzi Mtendaji wa Kamati ya Kimataifa ya Ushauri kuhusu zao la Pamba (International Cotton Advisory Committee -ICAC) ya hapa Marekani. Kwenye mazungumzo hayo, viongozi hao walijadili fursa za uwekezaji na kuimarisha ushirikiano kwenye kuboresha mnyororo wa thamani wa zao la pamba, ikiwemo uzalishaji wa bidhaa za nguo.
Tanzania ni nchi mwanachama wa ICAC na imekuwa ikinufaika na misaada ya kiufundi na fursa ya kujitangaza kwenye majukwaa ya uwekezaji yanayoandaliwa na taasisi hiyo. Mathalani, katika misaada ya kiufundi, mwezi Februari 2026, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Nguo (Textile Development) atafanya ziara nchini Tanzania ikiwa ni mwendelezo wa jitihada za kukuza uzalishaji wa nguo. Ikumbukwe kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zilizokuwa zinaongoza kwa uuzaji wa nguo hapa Marekani chini ya programu ya AGOA. Bidhaa za nguo kutoka Tanzania zilikuwa ni takribani asilimia 95 ya thamani ya mauzo ya bidhaa zote za Tanzania zilizokuwa zinanufaika na programu hiyo.

