Mheshimiwa Balozi Dkt. Elsie S. Kanza amekutana kwa mazungumzo na Dkt. Zarau W. Kibwe, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia, Kundi la Kwanza la Benki ya Dunia Kanda ya Afrika (World Bank’s Africa Group 1 Constituency). Mazungumzo hayo yalilenga kujadili masuala ya kipaumbele katika kudumisha uhusiano mzuri na wa muda mrefu uliopo baina ya Tanzania na Benki ya Benki ya Dunia. Uhusiano huo mzuri umeiwezesha Tanzania kuwa nchi ya pili kwa kunufaika zaidi na misaada na mikopo ya masharti nafuu inayotolewa na Benki hiyo kwa nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa na Sahara.  

Kwenye mazungumzo hayo, Viongozi hao walijadili namna bora ya kufungamanisha vipaumbele vya pande zote mbili, fursa zilizopo, ushiriki wa Tanzania kwenye mikutano ya kimuundo na mashauriano ya kimkakati na viongozi waandamizi wa Benki ya Dunia ili kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kunufaika zaidi.