Katika mwendelezo wa mazungumzo na wadau mbalimbali muhimu katika kukuza uhusiano baina ya Tanzania na Marekani, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alikutana kwa mazungumzo na Mhe. Jonathan L. Jackson, Mbunge wa Bunge la Wawakilishi la Marekani ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Ndogo ya Afrika ya Bunge hilo.
Pamoja na kujadili umuhimu wa kukuza uhusiano baina ya nchi hizo mbili, Mhe. Jackson alieleza pia dhamira yake ya kutembelea Tanzania kwa ajili ya kufahamu mambo mengi zaidi kuhusu nchi, watu wake, historia yake, vivutio vyake na utamaduni wake.
Baada ya Mkutano huo muhimu, Mhe. Waziri alifanya mazungumzo na baadhi ya kampuni za Marekani zilizowekeza Tanzania pamoja uongozi wa Chama cha Wafanyabiashara wa Marekani (U.S. Chamber of Commerce) na kujadili masuala yanayohusu kuimarisha uhusiano wa kibiashara baina ya Tanzania na Marekani.



